Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Tetesi za soka Ulaya

Everton wanajipanga kutoa dau la £60 milioni kwa ajili ya mshambuliaji wa Borussia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang, kimedai Mirror .
Toffees wamekuwa kwenye wakati mgumu msimu huu baada ya kushindwa kuziba pengo la mshambuliaji wa kati Romelu Lukaku.

Inter wapo tayari kupigana vikumbo na Juventus kwa ajili ya saini ya mchezaji wa Liverpool Emre Can, kwa mujibu wa
Tuttosport .
Kiungo huyo atakuwa amemaliza mkataba wake Anfield mwisho wa msimu huu na alikuwa karibu kutua Turin majira ya joto.

Real Madrid wamewasiliana na mshambuliaji wa Chelsea Eden Hazard kuangalia uwezekano wa kumleta Mbelgiji huyo Hispania kwa mujibu wa
Diario Gol .
Mchezaji huyo anasita kusaini mkataba mpya Stamford Bridge na ameeleza jinsi anavyoihusudu Real Madrid.

Arsenal wanakaribia kukamilisha usajili wa kiungo wa Schalke Leon Goretzka na watampata kama mchezaji huru, kwa mujibu wa The Sun .
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani atakuwa amemaliza mkataba wake mwisho wa msimu huu na yupo huru kuzungumza na klabu nyingine Januari, Arsenal nao wakiwa kwenye foleni.

Barcelona wapo tayari kutoa kitita cha £127 milioni kwa ajili ya kiungo wa Liverpool Philippe Coutinho dirisha la uhamisho la Januari, kwa mujibu wa
Mundo Deportivo .
Miamba hao wa La Liga hawakuweza kukamilisha dili dirisha la majira ya joto, lakini Mbrazili huyo bado ni chaguo lao namba moja.

Manchester City wapo tayari kutoa ofa nono kumsajili Alexis Sanchez kutoka Arsenal dirisha la uhamisho wa majira ya baridi Januari, kwa mujibu wa
Independent .
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Chile alikaribia kujiunga na kikosi cha Pep Guardiola majira ya joto, na mkataba wake utafikia mwisho ifikapo Juni 2018, City wanatarajiwa kutoa paundi milioni 50 kumsajili nyota huyo.

Everton wanamfikiria Theo Walcott kama mrithi sahihi wa Romelu Lukaku na wameshaanza mazungumzo na Arsenal kuhusu uwezekano wa kumpata mshambuliaji huyo, kwa mujibu wa Daily Mail .
Lukaku aliondoka Goodison Park kwenda Manchester United kwa kitita cha £75 milioni majira ya joto na pengo lake halijazibwa hadi sasa.
Inasemekana Walcott yupo sokoni Januari baada ya kushindwa kupata nafasi kikosi cha kwanza Arsenal msimu huu, na ni shabaha ya bosi mpya wa Everton Sam Allardyce.

Maoni